Maana ya jina Lunodzo (Andiko la kimtazamo)

Lunodzo Mwinuka
5 min readDec 7, 2023

--

Kwa kawaida binadamu ameumbwa na shauku ya kujua utambulisho wake katika nyanja mbalimbali. Moja kati ya shauku niliyokuwa nayo (bado ninayo) ni kujua maana halisi ya jina Lunodzo, ambalo ndilo nililopewa na wazazi wangu.

Mimi naitwa Lunodzo Mwinuka. Nimekuwa nikiitwa Luno (kama kifupisho cha Lunodzo) kwa miaka mingi kabla ya kuanza kutumia jina rasmi la Lunodzo kwa marefu yake katika nyaraka rasmi, hasa shule. Jina Luno halikushitua sana, na halikuniletea maswali mengi kama ilivyokuwa kwa jina Lunodzo kwakuwa jina la Luno tayari linatumika kwa kiasi kikubwa duniani kote (pesa za mitandaoni, majina ya kampuni, na majina ya watu). Kwa kifupi ni jina linalotumika katika mataifa mbalimbali na hata katika makabila mengine ndani ya Afrika.

Nini maana yake?

Lunodzo ni moja kati ya majina ya kibena ambalo hupewa mtoto wa kiume. Dhana ya halisi ya maana hutofautiana kulingana na matumizi, fikra au jamii ndani ya jamii za kibena. Pamekuwa na maelezo tofauti ya maana ya Lunodzo kutokana na uhalisia kwamba maana yake inatokana na hisia. Ikumbukwe kwamba, hakuna namna sahihi ya kuelezea hisia, kwa kawaida tunakuwa na maneno jumuishi kama furaha, upendo, chuki, majonzi, n.k. Kwa mfano, kila unapokula kitu kitamu, maelezo sahihi huwa ni matamshi kwamba “kitu -hicho ni kitamu”, ni vigumu kueleza ladha halisi hasa ukikosa kitu cha kufananisha ladha. Katika “uswahili” mara nyingi utamu hulinganishwa na vitu kama sukari na asali, uchachu hulinganishwa na vitu kama limao na ndimu, uchungu hulinganishwa na madawa (mnakumbuka lu(m)kalifya?). Huenda jina Lunodzo linadondokea kwa makundi ya maneno yanayoleta ugumu wa kutoa maana ya moja kwa moja ila linaweza kuelezewa kihisia.

Niliwahi kuhoji kwa wazazi wangu juu ya maana halisi ya jina langu. Na mara kadhaa nimeshuhudia kigugumizi chao, si katika mlengo wa kutokujua maana ila katika mlengo wa kutafuta neno sahihi la kuvalisha maana sahihi ya Lunodzo. Hivyo mara zote napata majibu ya “...ni kama kupendezesha”, “…ni kama upendo, lakini sio upendo sasa”, zikiambatana na maelezo ya mifano kadhaa ya maana ya Lunodzo. Moja kati ya sentensi iliyowahi kujirudia ni “Lunodzo lwa nguluvi/Ulunodzo lwa nguluve”, ikitafsiriwa katika maana isiyo rasmi kuwa “Upendo wa Mungu”. Dhana yangu ni kwamba, huenda kuna hisia wazazi wangu walikuwa nazo wakati wananipa jina hili, ambazo bado hawajawa tayari kuniambia au huenda sijahoji vema.

Mara kadhaa nimekuwa nikiambiwa maana ya Lunodzo kutokana na vitenzi vingine vya kibena kama “hunodza”. Hunodza (katika maana niliyoipata kutoka katika kutazama vitendo) ni kitendo cha kubusu mikono (iliyoshikana) wakati wa kusalimiana. Kitendo hiki kimezoeleka baina ya wabena na hufanyika na watu wawili wanaosalimiana kwa kushikana mikono. Kila mmoja hubusu (mikono iliyoshikana) kwa kupeana zamu (tazama picha hapo chini). Mama mkubwa (bibi wa mama), wakati wa uhai wake alinifunza hili kwa vitendo. Sijawahi shuhudia ndugu zangu wengine wakifanya hili. Hii ni hatari ya kupotea tamaduni za salamu za kibena.

Hunodza katika salamu ya kibena (Picha hizi zimetengenezwa na AI, kuelezeka kwa picha maelezo hapo juu na si vinginevyo)

Katika upande mwingine, sikuwahi kupata maana kutoka katika wazungumzaji walio wengi wa lugha ya kibena (kutoka katika makundi ya vijana niliokua nao). Wengi walionyesha kutokuwa na uhakika na maana ya moja kwa moja au kutofahamu kabisa. Wapo waliosema maana yake ni kupendezewa, kupendezesha, kupendeza, uzuri, n.k. Ambapo katika kila maana iliyotolewa mara nyingi palikuwepo na neno jingine la kibena lenye maana hiyo. Mfano, neno — pendez — likilinganishwa na — nogel — , pendeza = nogela, pendezesha = nogeledza. Yote yakitokana na neno la lunogelo.

Mmoja wa marafiki zangu ambao huwa napenda kuwauliza maswali juu ya lugha ya kibena, Bw. Stephano Kiwone (mwenyeji wa Kijiji cha Kanamalenga, Kata ya Ilembula), nilipomuuliza maana ya Lunodzo alisema,

…lina maana nzuri ila ni pana kidogo. Kama nyumba ni finishing.../pendezesha/koleza /mfano, winodza ikimaanisha kuremba. Pana misamiati mingi inaweza kuingia hapo lakini yote ina maana moja ya uboreshaji.

Kwa namna yoyote nilidhani Stephano atakuwa fundi ujenzi kwa sasa (kwahivyo nilihoji), lakini sivyo, japokuwa alishawahi kufanya shughuli za ujenzi kwa kiasi (hapa nilitaka kujifunza kama matumizi ya jina Lunodzo yanakuja kihisia zaidi kutoka na namna tunajisikia, au mapito tuliyopitia). Stephano alisema kwamba huu ulikuwa mfano rahisi wa kunielewesha.

Sambamba na hili, nilihoji suala hili pia kwa Bw. Rev. Isaac Chengula, naye alikuwa na haya ya kusema,

Si rahisi sana kupata tafsiri yenye kionjo halisi cha Lunodzo iliyomo ndani ya kibena chenyewe. Ila lina maana ya kitu/mtu chenye/mwenye sifa ya nakshisha/pendezesha/boresha/koleza kufikia kiwango murua/maridadi. Kifupi, fikisha kiwango cha mguso sahihi.

Maana ambayo binafsi yangu ilikata shauku ya kuendelea kupekua kwa maana ya kuridhishwa na majibu yaliyopatikana. Maana hii ilionekana kujumuisha yale yote niliyoandika huko juu.

Katika upande wa maandiko na tafiti za juujuu kupitia intaneti, jina Lunodzo limeelezewa na Bw. Mnata Resani katika andiko aliloliita “Maana katika Majina ya Wabena nchini Tanzania”. Mnata ameelezea majina mengi ya kibena yakiwemo majina ya Lutengamaso, Lunyamadzo, Anjendile, Twihuvila, Mutataluvanja na mengineyo mengi. Majina haya hutokana na mambo mbalimbali ndani ya jamii za kibena. Mnata amechambua majina kutokana na shughuli za kiuchumi, kuzaliwa nje ya ndoa, kuzaliwa baada na majonzi, upekee katika familia, historia, mtoto aliyezaliwa na mama alidhaniwa hatozaa, mtoto aliyezaliwa ugenini, majina kutokana na sifa za wazazi pamoja na mambo mengine.

Kwa mujibu wa Mnata, Lunodzo linadondokea katika kundi la majina yanayotokana na sifa ya mzazi. Katika kundi hili kuna majina kama Mpingwa, ambalo humaanisha mtu ambaye hana shida ya chakula, fedha za matumizi na mwenye tabia ya kutoa misaada kwa wenye shida. Majina katika kundi hili hupewa watoto wa kiume ambao wamezaliwa katika familia tajiri na ambao katika jamii yao ikitokea kuna tatizo hujitolea kwa misaada kuwasaidia wengine. Katika jamii za kibena majina haya yanatukumbusha kwamba ikitokea mtoto huyo akapata tatizo basi asaidiwe na mtu yeyote kwa kuwa wazazi wake waliwasaidia pia watu wengine wakati wa shida. Pia, jina la Amodzidze lina maana hiyo hiyo; ni visawe vya jina hilo. Hivyo kundi hili lina majina Mpingwa, Lunodzo na Amodzidze, yakijumuishwa na visawe vyake.

Mimi ni Lunodzo nyevaa…

Elimu haina mwisho, unaweza endeleza upekuzi wa maana za majina ya kibena likiwepo jina la Lunodzo kwa kupendekeza vyanzo mbalimbali katika mjadala hapo chini. Nini mtazamo wako?

--

--

No responses yet