Njombe si chafu kwa kiwango hiki!

Lunodzo Mwinuka
5 min readOct 21, 2023

--

Mama na kaka yangu wakifanya shughuli za shamba.
Mama na Kaka yangu, wakiwa katika shughuli za shamba, Ilembula.

Tumefika katika wakati ambapo uandishi wa habari na usambazaji wake unategemea “internet” huku idadi ya watumiaji ikiongezeka. Hii ni nzuri kwa vyombo vya habari, na watuamiaji wa habari. Kwa muda sasa, pamekuwa na habari nyingi (kwa mtiririko wa angalau habari moja kwa wiki) kutoka Njombe, huku 90% (makadirio) ya habari hizo zikiwa ni habari hasi zikiandika juu ya ubakaji, mauaji, hukumu za mahakama na mengine ya kufanana. Wakati nikikubali kwamba, ni kweli matukio haya yanatokea Njombe (pamoja na pembe nyingine zote za Tanzania), watumiaji wa habari hasa katika mitandao ya kijamii, wananyimwa haki ya kufahamu mambo mema yaliyopo Njombe. NJOMBE SIO CHAFU KWA KIWANGO HICHO!

Kuweka rekodi sawa, mimi ni mzaliwa wa Ilembula, Wilaya ya Wanging’ombe, Mkoa wa Njombe, na ninaandika haya kwa maslahi ya taswira ya Njombe (na ndugu zangu wa Iringa kwa kiasi), ingawa wang’amuzi wa mambo wanaweza kutumia jicho kubwa zaidi kupata picha ya mbali.

Kabla sijaenda mbali, niwakumbushe kwamba, kwa mujibu wa takwimu za hali ya Uhalifu na Matukio ya Usalama wa barabarani ya mwaka 2020 (Tanzania nzima), ubakaji ndio tukio lililoongoza kwa idadi ya makosa likiwa na jumla ya matukio 7,263, ikifuatiwa na mauaji, yenye matukio 2,225, na ulawiti yenye matukio 1,205. Matukio mengine katika kipengele cha Makosa dhidi ya binadamu ni wizi wa watoto, kutupa watoto, unajisi na usafirishaji haramu wa binadamu, yote haya yakiwa na jumla ya matukio 308. Hivyo kitaifa, ubakaji unaongoza ukiwa na 66%, mauaji 20.2%, ulawiti 11% na 2.8% kwa mengineyo katika matukio yote.

Katika makosa dhidi ya binadamu, mikoa (ya kipolisi) inayoongoza kwa idadi ya matukio ni Kinondoni (637), Dodoma (608), Kilimanjaro (606), Tanga (546), Mbeya (507), Kigoma (456), Morogoro (452), Ilala (438), Kagera (421), Tabora (409), Njombe (408). Katika haya, mkoa unaoongoza kwa mauaji ni Kagera na Tabora, ikiwa na idadi ya 163 na 152 kila mmoja. Mikoa inayoongoza kwa ubakaji ni Tanga (431), Kilimanjaro (418), na Kinondoni (381). Kiujumla, juu ya Njombe kuna mikoa kumi na moja (11) inayoongoza kwa idadi ya matukio ya aina hii. Tushangae pamoja.

Kwanini Njombe ing’ae katika vyombo vya habari?

Wakati likiwa ni swali lisilohitaji majibu ya aina ya ndio au hapana, ni dhahiri kwamba, huenda katika vyombo vya habari, hizi ndio habari ambazo zina uzika zaidi. Kwa namna yoyote, waandishi waliopo Njombe ndio chanzo cha habari hizi. Inashangaza kuona kwamba, panapotokeza matukio mawili makubwa ndani ya Njombe, mfano, ubakaji pamoja na kongamano la kilimo, vyombo vya habari kuchagua ubakaji kuliko kongamano la kilimo. Kwa muktadha huu, tuna wajibu wa kutafakari upya, lengo na dhumuni la habari katika taifa letu (Au Njombe tu?).

Nini vyombo vya habari haviwaambii kuhusu Njombe?

Pamoja na yote tunayoyasikia kwenye vyombo vya habari, ninajua kwa hakika kabisa Njombe kuna mengi mema ya kuwafaa Watanzania. Si kwa sababu nimezaliwa huko, ila kwa sababu ya yale ninayo yasoma nikiwa mbali na Njombe. Naleta fursa kadhaa nilizowahi sikia na kusoma mitandaoni, fursa ambazo vyombo vya habari aidha kwa makusudi au kwa sababu za kibiashara wameamua kuzitenga mbali na Watanzania.

KILIMO

Moja kati ya mashamba yaliyopo Madeke, Njombe.

Mkoa wa Njombe una hekari nyingi zinazofaa kwa Kilimo na yako maeneo ambayo serikali inayatenga kwa mpango maalumu, ikiwemo mradi mkubwa wa Ikang’asi ambao utagusa kilimo, viwanda, ufugaji na utalii.

Mkoa wa Njombe una hali nzuri ya hewa ambayo iko katika Kanda kuu tatu ambazo zinaweza kustawisha mazao mbalimbali kama ifuatavyo:-

Ukanda wa chini: Ukanda huu hulimwa mazao ya Mhogo, Mpunga, Karanga, viazi vitamu, korosho, Mtama, mbogamboga, matunda ya ukanda wa joto na migomba.

Ukanda wa kati: Mazao yanayostawi katika Ukanda wa Kati ni Mahindi, Maua, Maharage, Alizeti, Njegere, Migomba, Ngano, Viazi mviringo, Mbogamboga, Chai, Kahawa, Pareto na Matunda.

Ukanda wa Juu: Ukanda huu hulima mazao makuu ya Chakula ya Mahindi, Maharage, Viazi mviringo, ngano, njegere, alizeti, mbogamboga na matunda ya ukanda wa baridi, kwa Mazao ya biashara ni Chai, Kahawa, Pareto na Ngano.

Mkoa wa Njombe una ukubwa eneo la kilomita za mraba 24,994. Eneo linalofaa kwa kilimo ni hekta 1,090,000 na kati ya hiyo eneo lililolimwa kwa msimu 2017/18 ni hekta 374,637 sawa asilimia 34% ya eneo linalofaa kwa kilimo.

Fursa za uwekezaji katika uzalishaji mazao.

1. Uwekezaji katika uzalishaji wa mbegu bora za viazi mviringo.
2. Uwekezaji kwenye miundombinu ya uchunguzi wa afya udongo.
3. Uwekezaji katika ujenzi wa maghala na usambazaji wa pembejeo za kilimo hasa maeneo ya vijijini.
4. Uwekezaji katika usindikaji wa mazao ya mahindi kwa ajili ya unga na alizeti kwa ajili ya mafuta.
5. Uwekezaji katika uzalishaji wa zao la Parachichi.

Pamoja na mazao, Njombe pia kuna fursa za uwekezaji katika mifugo, samaki na misitu.

UTALII

Kitulo National Park

Njombe kunafanyika shughuli za utalii katika wilaya zake zote. Kwa kifupi, unaweza kupata maporomoko ya maji, makumbusho, misitu yenye mvuto wa asili na maajabu ya kuvutia, ngoma na nyimbo za asili, wanyama pori, utalii wa kilimo, “Matema Beach na Ziwa Nyasa, upande wa Ludewa”, mbuga za wanyama, Uwindaji, makaburi ya wapiganaji wa vita ya majimaji. Njombe pia kuna shughuli za uchimbaji wa madini.

Moja kati ya barabara za kuelekea Wilaya ya Ludewa.

Taarifa hizi zinapatikana pia katika tovuti ya Mkoa wa Njombe na Wikipedia.

Nitoe wito kwa waandishi wote waliopo Njombe, badala ya kuuza habari hizo mnazouza zaidi, washirikisheni Watanzania juu ya fursa na mazuri yaliyopo Njombe. Ninavyofahamu mimi, Njombe kuna “uchumi mkubwa”, hivyo kutoa fursa kwa Mtanzania yeyote kuweza kuishi na kuendesha shughuli zake za kiuchumi bila kuwa na changamoto ya kuhitaji pesa nyingi. Ni kweli kwamba hatuwezi kuandika kila kitu, ila tunaweza andika habari za kutujenga, kuliko habari za kutujaza masononeko na hofu juu ya uwekezaji.

Mwisho, niweke wazi tu kwamba, si kila chombo cha habari kimefanya hivi, na si kila mwandishi wa habari aliyopo Njombe, amefanya, tunao baadhi ambao, nadhani wanaweza kujirekebisha na kuandika habari njema kuhusu Njombe pia, bila kuzuia hizi zinazoendelea sasa.

Nawatakieni heri na amani wote.

Lunodzo.

--

--

No responses yet